Jumamosi 22 Novemba 2025 - 23:15
Kamanda wa Jeshi la Lebanon: Tuko Katika Hatua ya Kuamua Mustakbaki Wakati Uvamizi wa Ardhi ya Lebanon Ukiendelezwa na Israel

Hawza/ Jenerali Rudolf Haykal ametangaza kuwa Lebanon, katika mazingira ya kuendelea kwa uvamizi wa ardhi zake unaofanywa na Israel, inakabiliwa na moja ya hatua ngumu zaidi katika historia yake.

Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Jenerali Rudolf Haykal, Kamanda wa Jeshi la Lebanon, ametangaza kuwa Lebanon, katika kivuli cha kuendelea kwa uvamizi wa ardhi zake unaofanywa na Israel na mashambulizi yanayoendelea dhidi yake, imo katika moja ya hatua ngumu zaidi katika historia yake.

Jenerali Haykal, katika ujumbe wake kutokana na mnasaba wa maadhimisho ya mwaka wa themanini na mbili wa Uhuru, alieleza kuwa tangia kutekelezwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano, jeshi – licha ya uwezo mdogo na matatizo yanayotokana na mgogoro – limefanya juhudi kubwa kutekeleza mpango uliopitishwa, kuimarisha uwekaji wa majeshi katika upande wa kusini wa Mto Litani, na kupanua mamlaka ya serikali katika ardhi zake zote; sambamba na kushikamana kikamilifu na Azimio namba 1701 na utekelezaji wa vifungu vyake vyote, pamoja na uratibu wa karibu na Vikosi vya Muda vya Umoja wa Mataifa nchini Lebanon (UNIFIL) na Kamati ya Usimamizi wa Kusitisha Mapigano.

Akasema pia kwamba taasisi ya kijeshi imejitolea sana; baadhi ya wanajeshi wake wamepata shahada au kujeruhiwa wakilitetea taifa, huku wakiwa wamesimama imara katika ngome zao kuilinda haki ya Lebanon juu ya kila shubiri ya ardhi yake. Jeshi, katika njia hii, halitasita kutoa juhudi yoyote au tone lolote la damu, sambamba na kuunga mkono kurejea kwa wakimbizi vijijini mwao.

Kamanda wa jeshi alisisitiza kuwa juhudi hizi zinahitaji ushirikiano wa karibu kutoka kwa taasisi za serikali katika muktadha wa juhudi za kitaifa za pamoja, kupitia kuweka vifaa vinavyohitajika, kuboresha hali ya wanajeshi, na kuandaa mazingira yanayofaa kwa kurejea utulivu.

Akaongeza kuwa: “Uongozi unafahamu kikamilifu mazingira ya kipekee yanayoandamana na utekelezaji wa mpango wa jeshi, kama ambavyo unatambua kuwa hatua hii inahitaji kiwango cha juu cha busara, tafakuri, uthabiti wa maamuzi na ufanisi wa kitaalamu, ili kuhakikisha maslahi ya kitaifa na kulinda amani ya ndani bila kuzingatia hesabu zozote nyingine.”

Jenerali Haykal akiwahutubia wanajeshi alisema: “Shikamaneni na thamani zenu za kitaifa na muwe walinzi wa amani na utulivu wa taifa. Jueni kwamba jeshi ni kama jengo thabiti linalochukua nguvu yake kutoka kwa nguvu ya wanajeshi wake wote, na linasimama imara kupitia uthabiti wao. Kuweni thabiti katika kutekeleza wajibu wenu, na msijali kampeni za kutia shaka, kashfa na uvumi, na jueni kuwa ninyi daima mko upande wa haki.”

Na akiwahutubia wananchi wa Lebanon alisema: “Kama tulivyotarajia siku zote, bakini upande wa jeshi lenu, kwani jeshi lenu ndilo ngao yenu wakati mgumu. Imani yenu kwa taasisi ya kijeshi ndiyo msingi wa kuendelea kwake, na umoja wa ndani unaendelea kuwa nguzo kuu ya maendeleo ya Lebanon.”

Alimaliza hotuba yake kwa kusema: “Katika siku ya Uhuru, tunaboresha upya imani yetu kwa Lebanon na tunawakumbuka kwa heshima na utukufu mashahidi wetu waliotoa nafsi zao. Tunasisitiza kuwa changamoto, hata ziwe kubwa kiasi gani, haziwezi kuishinda azma yetu, na kuwa taifa letu, kwa baraka ya umoja wa watoto wake na uimara wa jeshi lake, litapita katika hatua hii.”

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha